3 Machi 2015 - 13:08
 Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine yuko Japan

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Pavlo Klimkin ameonesha wasi wasi wake leo kuhusiana na matarajio kwamba makubaliano yanayoungwa mkono

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ukraine  Pavlo Klimkin ameonesha  wasi  wasi  wake  leo  kuhusiana  na  matarajio kwamba  makubaliano  yanayoungwa  mkono  na  Umoja  wa Mataifa  ya  kusitisha  mapigano  na  waasi  wanaoiunga  mkono Urusi  yataendelea, wakati  akitoa  wito  wa  kupanuliwa  kwa  kikosi cha  kimataifa  cha kuangalia  makubaliano  hayo.

Klimkin  amewaambia  waandishi  habari  mjini  Tokyo  kwamba  hali katika  eneo  la  mapigano ni  mbaya  na  ya  wasi  wasi  licha  ya makubaliano  hayo. Amesema  bado  kuna  makombora  kadhaa yanavurumishwa  na  magaidi  mashariki  mwa  Ukraine.

Klimkin  ambaye  yuko Japan  kwa  mkutano  na  waziri  mkuu Shinzo  Abe pamoja  na  mwenzake  wa  Japan Fumio Kishida amesema  hayo  siku  moja  baada  ya  mawaziri  wa  mambo  ya kigeni  wa  Marekani  John Kerry  na  wa  Urusi Sergei Lavrov wameeleza  matumaini  ya  tahadhari  kufuatia  mazungumzo  yao mjini  Geneva  jana.

Wakati  huo  huo duru  katika  jeshi  la  Ukraine  zimesema  leo wanajeshi  watatu  wa  Ukraine  wameuwawa  na  wengine tisa wamejeruhiwa  katika  muda  wa  masaa  24  yaliyopita katika mapigano  na  waasi  mashariki  mwa  nchi  hiyo.